Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ameelekea nchini Bosnia na Herzegovina kufuatia mwaliko rasmi wa Rais wa Wanazuoni wa Kiislamu wa nchi hiyo, ili kushiriki katika “Hafla ya Mkataba” inayofanyika kwa ajili ya kuthibitisha rasmi uteuzi wa Rais wa Wanazuoni wa Kiislamu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika ziara hiyo ya siku tatu, mbali na kushiriki katika hafla ya kuthibitisha rasmi uteuzi huo, Ayatullah Arafi atakutana na viongozi mbalimbali wa kidini, kielimu na kisiasa, pamoja na kutembelea taasisi na vituo vya kitamaduni na kidini. Aidha, atakuwa na programu mbalimbali pamoja na Waislamu wa madhehebu ya Shia na Waislamu wengine nchini humo.
Katika ziara hiyo ya siku tatu, atakutana na Baqir Izetbegović, Rais wa zamani wa Bosnia na Herzegovina, ambaye ni mwana wa marehemu Ali Izetbegović, Rais wa kwanza wa nchi hiyo baada ya kupata uhuru, na kiongozi wa Chama cha Democratic Action. Pia atakutana na Šefik Džaferović, Rais wa zamani wa nchi hiyo; Sheikh Nedžad Grabus, Rais mpya wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Bosnia; Sheikh Husein Kavazović, Rais wa zamani wa Wanazuoni wa Kiislamu; pamoja na Sheikh Mustafa Cerić, aliyewahi kushika nafasi hiyo hapo awali.
Mbali na kutembelea taasisi zinazowakilisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Bosnia, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran atapata taarifa kuhusu shughuli za hivi karibuni zinazofanyika nchini humo, na kuchunguza fursa za kupanua ushirikiano kati ya Hawza na taasisi mbalimbali nchini Bosnia.
Aidha, Ayatullah Arafi anatarajiwa kufanya vikao maalumu na wasomi wabobezi katika nyanja za fikra na sayansi nchini Bosnia. Pia, katika mikusanyiko ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Waislamu wengine, atatoa hotuba kwa mnasaba wa kumbukumbu ya shahada ya Bibi Fatimah Zahra (s.a.), shahada ya Imam aliyeuawa kishahidi, pamoja na kusimulia ushindi uliopatikana katika vita viwili vya hivi karibuni.
Maoni yako